Friday, May 07, 2010

Mhadhiri Bakari Mohammed wa Mzumbe University amjibu JK kisayansi!

HOTUBA YA RAIS KIKWETE INA UPUNGUFU WA KISAYANSI

* Alitumia jazba, vitisho na kebehi
* Takwimu alizopewa ni “ghushi”
* Hakujibu madai mengine ya TUCTA


Kwa kuwa mantiki ni mtiririko wa hoja zilizopangwa ili kujenga hoja yenye kukubalika; na kwa kuwa sayansi ni elimu inayotokana na uchunguzi, majaribio, vipimo na kuthibitishwa kwa muda uliopo; kwa hiyo basi, hotuba nzuri ni ile inayozingatia kanuni za kisayansi kwa utumizi wa uchunguzi na mantiki. Sayansi lazima itumike kwa kuwa ndiyo inayoweza kuonesha ukweli na kuutenga na uwongo – uwe wa kimaslahi au vinginevyo – hotuba, kwa hivyo lazima isheheni ukweli na uhakika.

Makala haya nayaandika baada ya kuiskiliza hotuba ya Mhashimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyoitoa mbele ya wale waliyoitwa kuwa ni “Wazee wa Dar es Salaam” siku ya Jumanne tarehe 3 Mei, 2010 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee. Kwa ujumla, ilikuwa hotuba nzuri ya kisanii – kwa jinsi ilivyotumia lugha rasmi, mifano (mbayuwayu na kigong’ona) na vionjo vya lugha ya kwetu.

Mantiki ya jumla ya hotuba ya Rais Kikwete ilikuwa kuijibu TUCTA japokuwa alitumia nafasi hiyo kuzungumzia Mkutano wa Uchumi wa Dunia (World Economic Forum). Pamoja na mambo mengine ya utangulizi, sehemu muhimu na yenye kuhitaji upembuzi makini na wa kisayansi (uchunguzi + majaribio + vipimo + ithibati + mantiki) ni juu ya matumizi makubwa ya jazba, vitisho, kebehi na hisabati ghushi za takwimu zilizotumika katika kujibu hoja moja (kati ya tatu muhimu) zilizotolewa na TUCTA.

Rais Kikwete alitumia mfano wa “Mauwaji ya Wakata-miwa wa Kilombero” yaliyotokea miaka ya 1980 baada ya FFU (Kikosi cha Kutuliza Ghasia, maarufu kama fanya fujo uone) kutumia risasi za moto na kuuwa! Rais aliendelea kusherehesha juu ya madhila yanayoweza kutokea pale wafanyakazi watakapopambana na POLISI. Sidhani kama ni sahihi kudhani kuwa siku zote migomo huandamana na vurugu na/au ghasia zinazoweza kuzaa utumizi wa nguvu za ki-POLISI na hata mauwaji! Ulikuwa mfano mbaya kutoka kwa Kiongozi Mkuu wa Nchi, aliyesheheni “nguvu” za mamlaka ya kutumia vyombo vyote vya ulinzi na usalama. Ushahidi wa hili unajionesha wazi hata pale penye hadhara yenyewe (Diamond Jubilee): ulikuwapo uongozi wa (1) POLISI; (2) MAGEREZA; (3) Usalama wa Taifa; (4) JWTZ; na (5) Askari wa Siri (Secret Police). Kwa ujumla, mkutano ule ulipambwa na kila aina ya vitisho!

Japokuwa Rais ni Kiongozi wa Nchi na ana mamlaka ya kuamuru majeshi (Ibara ya 33(2), Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 [2005]) bado sayansi ya utawala haikubali kwa kiongozi muadilifu anayefuata haki na insafu kwa watu wake kutumia madaraka hayo dhidi ya utashi halali wa umma! Matumizi ya nguvu za ki-POLISI na/au kijeshi yamewahi kuziingiza nchi kadhaa kwenye sintofahamu na/au songombingo za kisiasa, kijamii na kiuchumi – kama tulivyoshuhudia Kyrgyzstan na tunavyoshuhudia sasa Thailand. Nguvu za ki-POLISI na/au kijeshi zitumike kwa hekima na si vitisho kwa raia (hususan wafanyakazi walalahoi – kama wakata-miwa).

Kwa upande wa utumizi wa lugha yenye murua – kiongozi yeyote awaye na mwenye mamlaka ya juu kiutendaji ana wajibu wa kuchagua maneno yenye hekima; kwa kuwa “hekima ni uhuru”! Rais Kikwete ametamka waziwazi kwamba, “…wafanyakazi wanaotaka kugoma waache kazi…kwa kuwa kuna watu wengi wanaohitaji kazi….” Ni ukweli usiyopingika kwamba “soko la ajira” Tanzania limefurika watu wanaotafuta kazi; lakini si kweli kwamba watu wote wanaotafuta kazi wana sifa stahiki kwa kila kazi.

Haitoshi, si kada zote za kazi (ziwe za kitaaluma na/au kimenejimenti) zina wazalendo wa kutosha kujaza nafasi zitakazoachwa wazi kutokana na: (1) wafanyakazi watakaouwawa (kama nguvu za ki-POLISI zitatumika); (2) watakaofutwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma; na (3) watakaoacha na kukimbilia ughaibuni [brain drain]. Nadhani hekima ilibidi itumike hapa ili wafanyakazi wasijione wanyonge mbele ya “Mwajiri Mkuu.” Naomba nichukue fursa hii kunukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere aliyoyatoa Dar es Salaam kwenye Sherehe za Mei Mosi mwaka 1974:


Tulipoanzisha vyama vya wafanyakazi, na halafu baada ya Uhuru kwa uamuzi wa Serikali ya TANU, wafanyakazi wa Tanzania wamelindwa wasinyonywe na matajiri wao, watu binafsi, na hata mashirika ya umma. Na ulinzi huo umezidishwa siku hata siku. Kima cha chini cha mishahara kimewekwa na kimekuwa kikiongezwa mara kwa mara. Sasa ni vigumu sana kumfukuza mfanyakazi, na kila mfanyakazi apate heshima yake kama binadamu (Julius K. Nyerere (1974): UHURU NI KAZI, National Printing Company Ltd, Dar es Salaam, ukurasa 15).

Nukuu hii inatufundisha msimamo wa Mwalimu Nyerere juu ya kuwahakikishia wafanyakazi: (1) ulinzi wa ajira zao dhidi ya unyonyaji unaofanywa na matajiri, watu binafsi, na mashirika ya umma (kama PPF); (2) kuweka kima cha chini cha mshahara na kukibadilishabadilisha kila mara kuendana na utashi wa mwendo wa kiuchumi; (3) kuondoa vitisho vya wafanyakazi kufukuzwa na waajiri; na (4) kuwapa wafanyakazi heshima yao kama binadamu [Ibara ya 12(2), Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 (2005)].

Hotuba ya Rais Kikwete imeonesha wazi kuwa leo wafanyakazi wa Tanzania si kama “Enzi za Mwalimu.” Soko la ajira la leo limewapa nafasi matajiri, watu binafsi, mashirika ya umma na Serikali (yenyewe) kunyonya jasho la wafanyakzai, kuendesha vitisho, kulipa mishahara isiyokidhi maisha (na mafao duni ya uzeeni na/au kiinua mgongo), vitisho vya kufukuzwa kazi, na ukosefu wa heshima kwa wafanyakazi! Inawezekana haya ni matunda ya kuliuwa Azimio la Arusha na mahala pake kuliweka “Azimio la Zanzibar!”

Ukiachilia mbali jazba, vitisho, na kebehi vilivyotumika kwenye hotuba hiyo kuna suala la utumizi wa takwimu ghushi (au ghashi). Kwa mujibu wa hotuba yenyewe (ambayo niliisikiliza mwanzo-mwisho), kutangazwa moja kwa moja (mubashara) na vituo vya runinga vya TBC1 na Star TV na kunukuliwa na magazeti kadhaa yakiwamo: Uhuru (ISSN 0876-3896, Namba 20553 la Jumanne tarehe 4 Mei, 2010); HabariLeo (ISSN 1821-570X, Namba 01230 la Jumanne tarehe 4 Mei, 2010); na Mwananchi (ISSN 0856-7573, Namba 03608 la Jumanne tarehe 4 Mei, 2010). Kwa pamoja, japo numerali (nambari) zilizotumika kwenye habari iliyonukuliwa ni tafauti, bado ukweli unabaki palepale juu ya takwimu zilizotumiwa na Mheshimiwa Rais kuwa ni ghushi.

Rais Kikwete, alitoa mfano kwamba Serikali ikitoa kiwango cha shilingi 315,000 (laki tatu na kumi tano elfu) za ki-Tanzania kwa kila mtumishi (mfanyakazi) itabidi iwalipe watumishi (wafanyakazi) zaidi ya 300,000 (laki tatu) wa sekta ya umma shilingi 6.9 trilioni (Mwananchi), shilingi 6.85 trilioni (Uhuru), na shilingi 6,852.93 bilioni (HabariLeo). Kwa ujumla, takwimu zote zilizonukuliwa zinaonesha kuwa gharama ya kuwalipa watumishi (wafanyakazi) wa Serikali wapatao 350,000 (laki tatu na hamsini elfu) hivi ni shilingi za ki-Tanzania trilioni 6.85293 (kwa mujibu wa gazeti la Serikali, HabariLeo). Takwimu hizo za gharama ya mishahara zilitumiwa na Rais Kikwete kulinganisha na makadirio ya mapato ya Serikali kwa mwaka 2010/2011 yanayokadiriwa kufikia trillion 5.7573 (kwa mujibu wa gazeti la Serikali, HabariLeo) na hivyo kuonesha nakisi ya bajeti ambapo Serikali itawajibika kukopa!

Ilinichukuwa muda kukaa na kutafakari juu ya “ukweli” huu wa ki-hisabati. Japokuwa hisabati ni tatizo la taifa, namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba nilipata bahati ya kusoma hisabati tangu nilipoanza kufundishwa hesabu za vidole hadi chuo kikuu! Ziwe hisabati za kikwetu (Traditional Mathematics), hisabati za Entebbe (Entebbe Mathematics), hisabati za msingi (Basic Mathematics), hisabati za ziada (Additional Mathematics), hisabati za juu (Advance Mathematics) hata hisabati halisi (Pure Mathematics) haziwezi kukubaliana na udondozi wa ki-takwimu uliyotumiwa kurahisha hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Rais! Na tutumie mifano ili kuelezea hoja ya ki-hisabati kwa utumizi wa sayansi ya nambari (observation + logic).

Achilia mbali wafanyakazi 350,000 (laki tatu na hamsini elfu), tuchukue Serikali ina watumishi (wafanyakazi) 400,000 (laki nne). Angalia jedwali lifuatalo jinsi ya udondozi na/au ukokotozi wa kihisabati:


KIKOKOTOZI GHARAMA


IDADI YA WATUMISHI (iliyokadiriwa)


MSHAHARA KWA MWEZI + Bima + Akiba


IDADI YA MIEZI KWA MWAKA


GHARAMA

Mshahara
400,000
315,000.00

12


1,512,000,000,000.00

Akiba (Mifuko ya Hifadhi ya Jamii)
400,000
315,000.00 (15%)

12


226,800,000,000.00

Bima ya Afya
400,000
315,000.00 (3%)

12


45,360,000,000.00

JUMLA
400,000
371,70.00

12


1,783,160,000,000.00



Kama tukichukuwa mshahara kama “kikokotozi cha gharama” pasipokuwapo na 15% ya akiba (kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii – PPF, PSPF, LAPF na NSSF) na 3% ya bima ya afya (NHIF) serikali itatumia shilingi 1.512 trilioni! Huu ni ukweli wa kihisabati kama wafanyakazi 400,000 (laki nne) watalipwa kima cha chini cha mshahara wa shilingi 315,000 (laki tatu na kumi na tano elfu) Serikali itagharamia shilingi trilioni 1.512 na si shilingi trillion 6.85293! Na hata kama tutachukuwa akiba (15%) na bima (3%) ya afya kwa pamoja (na gharama za huduma nyingine – OC) bado gharama haiwezi kuzidi trilioni 2! Huu ni ukweli wa ki-hisabati na si vinginevyo. Kosa kubwa la kihisabati lililofanywa hapa ni kama asilimia 74 (74%) kutoka kwenye ukweli – hili ni kosa kubwa ki-hisabati – ni mara tatu hivi kutoka kwenye gharama halisi!

Inawezekana Mheshimiwa Rais alipewa takwimu ghushi ili kuonesha kuwa watumishi (wafanyakazi) wa Serikali hawana uzalendo kwa kudai mishahara “mikubwa” kuliko uwezo wa Serikali kugharamia mishahara hiyo! Kama ni kweli alipewa takwimu ghushi, basi aliyempa (na/au waliyempa) wanastahili “adhabu” stahiki kwa vile takwimu hizo ndizo zilizomfanya Mheshimiwa Rais kuhamaki na kupandwa na jazba na hata kutoa vitisho na lugha ya kebehi kwa wafanyakazi. Watu wote waliyomdanganya Mheshimiwa Rais hawana budi kushughulikiwa ipasavyo – na kama ni wasomi wa vyuo vyetu vya ndani basi vyuo vilivyowatunuku stashahada na/au shahada hizo havina budi kuwanyang’anya – kwa vile wamempotosha Rais wa Nchi!

Jambo la mwisho kabla sijahitimisha makala haya nimalizie na nukta kwamba Mheshimiwa Rais hakujibu madai mengine “nyeti” na muhimu yaliyotolewa na TUCTA. Ni yale ya kodi kubwa ya mapato (inayotokana na mishahara) na mafao duni ya uzeeni yanayotolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii (hususan PPF). Si jambo jema kuukwepa ukweli japokuwa unasemwa na mtu anayeonekana “duni” na “dhalili.” Ukweli utabaki kuwa ni silaha ya jasiri na uwongo ni silaha ya mwoga! Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kuandika hivi:


Ukweli una tabia moja nzuri sana. Haujali mkubwa wala mdogo; haujali adui wala rafiki. Kwake watu wote ni sawa. Pia ukweli una tabia ya kujilipiza kisasi kama ukipuuzwa…. Ukweli haupendi kupuuzwa-puuzwa... Wakati mwngine, mtu tunayempinga huwa ana makosa kweli, lakini hoja tunazozitoa ni za ki(bi)nafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake. Nikisema mbili na tatu ni sita, nakosa. Lakini ni bora kunionesha kwamba pengine nafikiri tunazidisha kumbe tunajumlisha. Ni kweli mbili mara tatu ni sita; lakini mbili na tatu ni tano siyo sita…. Huu ni mfano wa upuuzi; lakini mara nyingi hoja tunazozitumia kuwashawishi watu wakatae mawazo yetu huwa hazihusiani kabisa na mambo tunayoyajadili (Nyerere, J. K (1962): TUJISAHIHISHE, Dar es Salaam, National Printing Company Ltd, ukurasa wa 3).


Nadhani ni wakati muafaka sasa tuukubali ukweli – hali za wafanyakazi wa Tanzania kwenye sekta ya umma na sekta ya binafsi zinahitaji marekebesho yenye dhamira nzuri – na si vitisho na/au utumizi wa takwimu zisizo na ukweli ili kuogopa kisasi cha ukweli. Mwalimu Nyerere aliliona hili na ndiyo maana aliamua kutuachia urithi wa kitabu hiki chenye umri wa miaka takriban sawa na Uhuru wa Tanganyika! Tujaribu kuyaangalia maneno haya ya Mwalimu Nyerere kwa kuyanukuu kama yalivyo:


Makosa ni makosa na dhuluma ni dhuluma, japo watendao makosa hayo au dhuluma ile ni wakubwa au ni wengi. Chama kinachopenda ukweli na haki hakina budi kiwape wanachama wake uhuru na nafasi ya kusahihisha makosa na kuondoa dhuluma. Wanachama hawana budi waone kuwa ni wajibu wao kuutumia uhuru huo, na nafasi hiyo. Wanachama wasiyotumia uhuru huo na nafasi hiyo, kwa sababu ya kuogopa kuchukiwa au kupoteza nafasi zao, wanafanya kosa kubwa la u(bi)nafsi, ambalo ni adui wa haki na ukweli (Nyerere, J. K (1962): TUJISAHIHISHE, Dar es Salaam, National Printing Company Ltd, ukurasa wa 5).


Haitakuwa vema na wala si haki tukiacha kusimamia ukweli. Ili kuogopa ukweli usijilipize kisasi (Nyerere, 1962) hatuna budi kama raia wa Tanzania kusimamia ukweli ili haki itendeke. Asiachwe mkubwa atende makosa huku wananchi wakimshangilia kwa nyimbo za “sema usiogope” na vigelegele vya tangazo la kuwafuta kazi watumishi watakaogoma! Tanzania ni ya Watanzania na itajengwa na Watanzania kama uongozi utazingatia haki, usawa na uadilifu katika matumizi bora ya rasilimali watu na vitu. Maendeleo ya watu hayaji isipokuwa kwa sera na siasa safi isiyokinzana na utashi wa ki-maumbile.

Sidhani kama kuna watumishi wa Serikali wenye kuona “gere” au kuwa na “hiyana” na CCM hata kutengeza “zengwe” lililoitwa agenda binafsi ya uchaguzi 2010! Wafanyakazi waliitumia Mei Mosi 2010 kutoa wito wao wa “Uchaguzi Mkuu 2010 uwe Suluhisho la Kero za Wafanyakazi.” Nadhani huu ni ukweli wafanyakazi wana kero zao pamoja na (1) mishahara isiyokidhi haja, (2) kodi kubwa ya mapato yatokanayo na mishahara, na (3) mafao duni ya uzeeni yanayotolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii (hususan PPF) – huu sio upinzani wa kisiasa na wala hauwezi kutumika kama “agenda ya siri” dhidi ya CCM. Tukumbuke Mwalimu Nyerere (1962) aliwahi kuandika hivi:


Pengine kundi “letu” ni sisi Wana TANU, na “lao” ni la wale wasiokuwa Wana TANU. Kwa mfano, baadhi ya Wana TANU husahau kabisa kuwa baadhi ya watumishi wa serikali ni wananchi safi kabisa kama sisi, na pengine kuwazidi wengine wetu. Lakini kwa sababu hawana kadi za TANU, basi, hufanywa kuwa si kitu. Pengine huongezeka kosa lile lile la kuwafanya wao kuwa ni watumishi tu ambao hawastahili heshima yoyote ya utu. Pengine, kwa sababu baadhi yao wanayo elimu nzuri, huongezeka kosa lile la kuwatilia mashaka wenye elimu. Sisemi kwamba huwa hawana budi wahukumiwe kwa makosa yao ya kweli, si kwa kubwagwa tu katika kundi la walaumiwa bila makosa yao wenyewe (Nyerere, J. K (1962): TUJISAHIHISHE, Dar es Salaam, National Printing Company Ltd, ukurasa wa 13).


Nukuu hii ni muhimu kwa wakati huu. Isitokezee Serikali ya CCM ikadhani kuwa watumishi safi ni wanaCCM pekee – hiyo itakuwa kuwahukumu watumishi wengine wasiyokuwa wanaCCM pasipo na haki. Hakuna haja ya kuwatilia mashaka wenye elimu kwa kuwa uzalendo haupimwi kwa kuwa na kadi ya “chama tawala” isipokuwa utumishi uliyotukuka! Mwisho tukumbuke kuwa, “kila raia anastahili fursa na haki sawa, kwa masharti ya usawa, ya kushika nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyo chini ya Mamlaka ya Nchi [Ibara 22(2), Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 (2005)].

Na asibaguliwe mtu kutokana na itikadi yake ya kidini, kisiasa, kiuchumi au kijamii. Na Mamlaka ya Nchi ihakikishe kuwa, “kila mtu anayefanya kazi (ya halali) kwenye sekta binafsi au ya umma anastahili kupata malipo ya haki [tazama Ibara 23(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 (2005)]. Mwenyezi Mungu Mtukufu azikunjue nafsi zetu na Atupe hekima ili tuwe huru na mawazo ya chuki dhidi wa watu wasiyo na hatia – na tunapohukumu basi tuhukumu kwa haki kwa kuzingatia usawa, insafu na uadilifu.


“TUMEONEWA KIASI CHA KUTOSHA, TUMENYONYWA KIASI CHA KUTOSHA, TUMEPUUZWA KIASI CHA KUTOSHA. UNYONGE WETU NDIO ULIOTUFANYA TUONEWE, TUNYONYWE NA KUPUUZWA. SASA TUNATAKA MAPINDUZI, MAPINDUZI YATAKAYOTUFANYA TUSIONEWE, TUSINYONYWE NA TUSIPUUZWE TENA,” (AZIMIO LA ARUSHA, 1967).



MUNGU IBARIKI TANZANIA WABARIKI NA WATANZANIA


Makala haya yameandikwa na:

Bakari M Mohamed
Mhadhiri Msaidizi
Kitivo cha Biashara,
Chuo Kikuu Mzumbe,
S.L.P 6,
Mzumbe – Tanzania.
Simu ya kiganjani: +255 713 593347
Barua pepe: maligwa1968@yahoo.com , bakari.mohamed@mzumbe.ac.tz