Tuesday, November 29, 2011

“POSHO SI DHAMBI , DHAMBI NI POSHO INAPOKOSA UTU” - LEMA


Nimetafakari sana niliposoma kwenye magazeti kuwa sisi wabunge tumeongezewa posho bila hata sisi kufahamu jambo hilo .
Na kila mtu ametoa maoni mbali mbali juu ya jambo hili , ni kweli ni msimamo wa chama chetu (Chadema) kupinga posho mbali mbali zisizokuwa na tija na tulikubaliana hivyo kwenye vikao vya Chama Chetu vya Wabunge na kupinga mfumo wa posho uliopo kwa sasa ni msingi sahihi wa Chama kuonyesha hisia na ubadhilifu mkubwa unaotokana na ulipwaji mbaya wa posho kama ambavyo imejitokeza mara nyingi na hata hivi karibuni tumeshuhudia madudu mengi kwenye ripoti ya kamati ndogo ya Bunge iliyomchunguza Jairo. Lakini suala hili haliwezi kuepukwa kabisa na Chama kinajua ila utaritibu wa ulipwaji posho kwa watumishi mbali mbali wa umma ni tatizo kubwa na kuna mapungufu mengi sana ndio maana kupinga posho haina maana tu ya kupinga kiwango cha pesa anachopokea Mbunge au mtumishi yeyote wa UMMA bali mfumo mzima wa sera ya posho ili uweze kuwa na tija na kupunguza mianya ya wizi katika mfumo huu ambao umekuwa ukitumika vibaya kuliibia Taifa.

Pengine sisi wabunge ni vyema tukatambua kwanini wananchi wanapiga kelele kuhusu posho nilishawahi kusema Bungeni wakati nachangia kwenye Wizara ya Ustawi wa Jamii kuwa mshahara wa Wabunge , posho mbali mbali za Wabunge pamoja na marupurupu mengine yanaonekana kuwa anasa pale watumishi wengine wa serikali kama Manesi ,Asikari Magereza,Polisi ,Makarani Mahakamani wanapolipwa chini ya shilingi laki mbili na nusu kwa mwezi na wakati huo huo wanasikia mwakilishi wao akipiga kelele Bungeni kuwa posho ya laki mbili kwa siku ni ndogo. Ndio maana nimesema “POSHO SIO DHAMBI ILA POSHO NI DHAMBI PALE POSHO INAPOKOSA UTU , Na hapa lazima kutokee ugomvi wa kimasilahi na mgogoro mkubwa kati ya mwakilishi na anaye wakilishwa.

Pengine masilahi anayopata Mbunge ni ya kawaida sana tena sana ila yanaonekana kuwa anasa pale ambapo yeye kama mwakilishi anapolipwa kiwango cha posho cha siku moja ambacho ni sawa na mshahara wa mpiga kura wake kwa siku thelasini. Mimi nafikiri namna peke ya wabunge kutetea masilahi yao bora kwanza ni kupigania masilahi ya wapiga kura wote Tanzania na tukifanya hivi kama Wabunge hakuna Mwananchi hatakayeshangaa kwanini Mbunge awe na masilahi bora kwani ubunge ni nafasi kubwa pia inayositahili heshima kubwa kwani ni uwakilishi katika jamii.

Ebu jiulize wananchi wanaposikia Wabunge wamepewa milioni tisini kununua magari na wakati huo huo serikali imenunua bajaji kuwa ndio magari ya kubeba wakinamama wajawazito yaani (Ambulance) ni wazi kabisa wabunge wataonekani ni watu katili na walioenda bungeni kwa masilahi binafsi japo kuwa ukweli unabaki kuwa Wabunge wanahitaji magari imara na mazuri. Lakini Wabunge kama watafikiri Bajaj ni sawa kuwa gari la wakinamama wajawazito na wao kuchukua milioni tisini kwa magari ya binafsi bila kupiga kelele na kukataa unyanyasaji huu kwa wakina mama na Wagojwa ,hivyo ni dhahiri kuwa ugomvi hapa katika posho na masilahi ya Wabunge utasababishwa na tofauti ya masilahi dhidi ya wale waliowachagua kuwatetea ,Hivyo namna pekee Mbunge anaweza kutetea masilahi yake bora bila kuingiliwa na na kubugudhiwa ni Mbunge kuanza kufikiria masilahi ya watu wengine ambao pia ni watumishi wa UMMA ambapo yeye ni mwakilishi wake .

Nafahamu kuwa pamoja na kupinga mfumo mzima wa utaritibu wa posho ulivyo sasa tafakari ya kweli ni kwamba masilahi ya watumishi wa UMMA bado ni madogo sana kwa hiyo Uzalendo wa kweli sio tu kupinga masilahi bora bali serikali iwajibike kikamilifu kudhibiti wizi na ufisadi unaotokana na utaritibu mbaya wa ulipwaji posho , kuongeza makusanyo katika kodi mbali mbali ,kutumia rasilimali za Nchi vizuri ili masilahi ya watu wote Nchi hii yaweze kuwa na tija kwa maisha ya Watanzania na watu wengi waweze kuishi maisha ya faraja na kutimiza malengo yao muhimu ya maisha
Ndio maana nimesema “POSHO SIO DHAMBI ILA POSHO NI DHAMBI PALE POSHO INAPOKOSA UTU.

Nitakuwa ni mtu mwenye mashaka sana kama nikiwaza kuwa masilahi duni na maisha ya kuishi chini ya kiwango ni Uzalendo , Sasa Wabunge mkitaka msipigwe mawe barabarani ,msitukanwe , msionekane ni wasaliti wa jamii aliyowachagua , Sasa huu ni wakati wakusema , Mshahara wa Polisi ,Magereza,JWTZ, Walimu, Makarani Mahakamani na hata sekta zote za Serikali na Binafsi masilahi ya mishahara yao yaongezwe kwa asilimia kama ambavyo mmjiongozea nyie kwenye posho zenu tena zinazohusu siku moja tu lakini wao wanaomba kwa mwezi lakini hawapati. Sasa pamoja na kupinga mfumo mzima wa sera ya posho kama ambavyo Mwenyekiti wetu wa Taifa alisisitiza na kuomba sera hii iangaliwe upya ili kupunguzia Taifa mzigo mkubwa na kuboresha viwango vya mishahara vya watumishi wa UMMA , ni vyema nikarudia kusema kuwa ““POSHO SIO DHAMBI ILA POSHO NI DHAMBI PALE POSHO INAPOKOSA UTU.

Ni kweli gharama za Maisha zimepanda lakini hazikupanda kwa Wabunge tu pia kwa Wananchi wote wanaoishi Tanzania , Hivyo tukiacha ubinafsi tukawajibika vizuri Bungeni kulinda masilahi ya Taifa na kutetea maisha ya Wananchi wetu, bila shaka hata tukionekana tunaendesha magari ya kifahari kama Rolls Royce, Bentley, Benz , hakuna mwananchi hatakeyesema kwa nini Mbunge anaendesha gari zuri kwani kila mtu atakuwa na afadhali ya maisha ktk Nchi yetu.

“ Baba yangu aliniambia “ Watu wengi wanaokwenda Kanisani na Misikitini huwa wanatoa sadaka ndogo kuliko pesa wanayotumia sehemu mbali mbali za anasa ndio maana Taifa lina Bar nyingi kuliko nyumba za Ibada” TAFAKARI

LEMA- MP

Thursday, November 24, 2011

AJALI MBAYA YA LORI DAR ES SALAAM



SIMANZI na majonzi jana vilitawala eneo la River Side, Dar es Salaam baada ya ajali mbaya iliyohusisha lori la mafuta na magari mengine madogo saba kusababisha vifo vya wawili papo hapo na wengine wanne kujeruhiwa vibaya. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa saba mchana na kwamba maiti na majeruhi wote walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Ilala, Amana.

Lori la mafuta aina ya Marcedes Benz la Kampuni ya Dalbit lililokuwa likielekea Buguruni liliacha njia na kuyagonga magari saba yaliyokuwa kwenye foleni ya kuelekea Ubungo. Magari mengine yaliyohusika katika ajali hiyo ni Toyota Noah, BMW, Toyota Canter na Toyota Corolla nne. Mmoja wa waliofariki dunia ni mama mmoja ambaye mwili wake ulitenganishwa kabisa na kichwa baada ya gari alilokuwemo kukandamizwa na lori hilo.

Habari kutoka eneo la tukio, zilieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni lori hilo kuacha njia, baada ya dereva wake kutaka kumkwepa mtembea kwa miguu ambaye alielezwa kuwa ni mama mjamzito. Watu hao wawili waliofariki dunia walikuwa kwenye magari tofauti.

Hata hivyo, habari nyingine zinadai kwamba miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo ni mchuuzi kanda za video ambaye alikuwa akitembeza biashara yake katika eneo hilo. Baadhi ya majeruhi walisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa lori hilo la mafuta baada ya dereva wake kushindwa kulimudu alipojaribu kumkwepa mtembea kwa miguu aliyekuwa anavuka barabara.

“Nilikuwa naelekea Ubungo nikiwa katika foleni, mara nikaona lori la mafuta likiwa linahama njia na kuja upande wetu. Baadaye kidogo, sikuelewa tena kilichokuwa kimetokea,” alisema Yahaya Makame.

Makame ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema licha ya kutokea kwa ajali hiyo mbaya, hakukuwa na msaada wowote wa haraka zaidi wa wakazi wa eneo hilo na wapita njia waliojitokeza kushuhudia. “Ajali imetokea saa 7:00 mchana, lakini, waokoaji wanafika saa 8:00.

Muda wote huo watu walikuwa bado wako ndani ya magari hayo wakiwa wameminywa na lori! Kuna usalama hapo kama siyo neema ya Mungu?” Gari la polisi liliwasili eneo la ajali majira ya saa nane mchana kusaidia uokoaji.

Tume ya katiba sio chombo cha serikali-Shivji


TANZANIA ipo katika vuguvugu la katiba mpya ambalo wiki iliyopita lilichukua sura mpya baada ya matakwa ya asasi za kiraia, wabunge wa vyama vya upinzani na wananchi kwa upande mwingine kupitia asasi za kiraia kupuuuzwa na serikali hivyo kuusoma muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba kwa mara ya pili kinyume na ilivyotakiwa.

Wanaharakati, upinzani na asasi za kiraia walikuwa na hoja ya kutaka muswada huo usomwe kwa mara ya kwanza kwa madai kuwa kuna marekebisho ambayo yamefanywa mara baada ya kusomwa mara ya kwanza na kuusoma kwa mara ya pili si kuwatendea haki wananchi.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu, Profesa Issa Shivji anasema kitendo cha serikali kuusoma kwa mara ya pili na kupuuza hoja za wadau wengine ni jambo lisilofaa na linaweza kuitumbukiza nchi katika matatizo yasiyo na msingi wowote.

Anasema kinachofanyika sasa ni sawa na kile ambacho kilifanyika mwaka 1977 chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa ambapo Rais wa kwanza, Julius Kambarage Nyerere alichagua Bunge la Katiba ambalo liliwashirikisha wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hakuna tofauti na wakati ule hivyo kuna hatari ya kupata katiba ambayo haina uhalali wa wananchi kwani itakuwa imetungwa na watu wachache hivyo sioni kwanini turudie makosa ya miaka 40 iliyopita, anasema.

Akichambua zaidi hoja yake hiyo, anasema kulingana na muswada huo Rais wa Bara atawachagua wajumbe wa tume 36 na ibara ya sita ya muswada huo inaeleza kuwa Rais atachagua wajumbe wengine kwa kutumia vigezo ambavyo vimetajwa baada ya makubaliano na Rais wa Zanzibar na ni pamoja na vile ambavyo Rais ataona vinafaa.

Shivji anasema hapo kuna utata kwani muswada haupo wazi kueleza Rais ataona inafaa vipi na hilo anasema ni kumpa madaraka makubwa kiongozi huyo wa nchi katika uteuzi wa tume hiyo ambayo kimsingi ni ya wananchi na sio ya chama, serikali wala kikundi kingine chochote.

Uteuzi wajumbe wa Tume
Kulingana na muswada huo, wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Baraza la Wawakilishi ambao wapo chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), watakuwa wajumbe wa Bunge hilo la katiba.

Wajumbe wengine wanatajwa kuwa ni mawaziri wa katiba wa serikali zote mbili (Bara/Zanzibar), wanasheria wa pande mbili, wajumbe kutoka mashirika 126 ambayo yameorodheswa na kwa hesabu za haraka Profesa Shivji anasema Bunge hilo litakuwa na wajumbe 554.

Profesa Shivji anasema mchanganuo unaonyesha kuwa wajumbe hao wa Bunge la Katiba kati yao 404 watakuwa wa CCM, 124 watatoka Zanzibar na idadi inayobaki ndio wadau wengine. Profesa Shivji anasema idadi hiyo ni kubwa na haiwezi kuleta ufanisi.
Sijui vipi, lakini India ambayo ina watu wapatao milioni 300 Bunge lao la Katiba mwaka 1945/46 lilikuwa na wajumbe 215 tu, anasema Profesa Shivji.

Swali la kujiuliza hivi wabunge wanaotajwa kuwapo katika Bunge la Katiba wanamwakilisha nani? Wananchi si wapo katika Bunge hilo la Katiba? Je, wao wapo kwa ajili ya nani?
Profesa Shivji anasema makundi hayo mawili yaliingia uwakilishi bungeni kwa mujibu wa katiba iliyopo na walienda huko kutunga sheria kwa mujibu wa katiba hiyo na sio kuipindua ili kuwa na katiba mpya hivyo haoni mantiki ya kuwapo kwao.

Mwenyekiti huyo wa Kigoda cha Mwalimu anahoji kuwapo kwa wabunge wa viti maalum wa CCM na wateule wengine kama asasi za kiraia kunatia wasiwasi na hata hizo NGO ambazo amezichagua Rais si vyombo vya uwakilishi wa wananchi.
NGO ni ‘pressure group’ (makundi ya kushinikiza), tusidanganyane na mara nyingi huwa zinawawakilisha wafadhili baadala ya wananchi. Profesa Shivji anauliza wapi ilipo nafasi ya wananchi katika Bunge hilo?

Aidha anasema kifungu kinachotaja kuwa Rais atateuwa wajumbe baada ya makubaliano na Rais wa Zanzibar ni kuhodhi madaraka ya wananchi.
Kifungu cha sita kimeweka vigezo ambavyo Rais atavitumia na maelezo kuwa na wengine watateuliwa kulingana na vigezo ambavyo rais ataona vinafaa kinajenga maswali zaidi kuliko majibu.

Hapo ni sawa na kumpa mtu kitu kwa mkono wa kushoto kisha kumnyang’anya kwa mkono wa kulia, anasema na kuongeza kuwa Rais kutoa hadidu za rejea za tume hiyo ni kuibaka demokrasia.

Hadidu za rejea
Kulingana na muswada huo, Profesa Shivji anasema kuwa hadidu za rejea zinatolewa na Rais kwa kukubaliana na kushauriana na Rais wa Zanzibar na kitu kama hicho kitafanyika pia katika uteuzi wa katibu wa sekretarieti ya Bunge hilo.
Wajumbe wa sekretarieti watateuliwa na Waziri wa Sheria ambaye pia ndiye mwenye dhamana ya kuwalipa na ndiye ambaye atajua kiwango cha posho na stahili zao zingine na baada ya tume kufanyakazi yake watayakabidhi mapendekezo kwa Rais.

Mapendekezo yatakabidhiwa kwa mujibu wa kifungu namba 18 (2) na baada ya kushauriana na mwenzake wa Zanzibar na baada ya kumaliza majadiliano ya sera na utendaji, Rais atamuagiza Waziri wa Sheria kuwasilisha katika Bunge.
Baada ya kupokea, atamuagiza waziri ayatangaze bungeni, je, akishapokea hataweza kubadili Sheria haimzuii anasema Profesa Shivji.

Shivji anasema anadiriki kusema kuwa ni tume ya marais wawili wa Zanzibar na Bara na sio ya katiba na anaeleza hatua ya kwanza katika kuiunda imewaacha wananchi kando hivyo kupotosha mchakato mzima.
Mwenyekiti huyo wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere anasema sekretarieti ni muhimu ni nani anaiteua ni jambo ambalo linahitaji umakinifu mkubwa na anatoa mfano wakati alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Sheria ya Ardhi wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi.

Nilipochaguliwa kuwa mwenyekii wa tume ya ardhi na kupewa ofisi Wizara ya Ardhi, sekretarieti ilikuwa itoke Wizara ya Ardhi, watumishi wa wizara ndio walikuwa sekretarieti, mkutano wa kwanza na wa pili tulioufanya, miniti za kikao hazikuchuliwa, hapo nikaona wazi kuwa tume haiwezi kufanyakazi.

Anasema aliona hivyo kutokana na ukweli kuwa huwezi kuwa na seretarieti kutoka wizarani ambao ndio wanaochunguzwa na tume jambo ambalo alililalamikia na kutakiwa kuchagua sekretarieti yake mwenyewe, hali ambayo ilimuwezesha kufanya kazi zake inavyotakikana.
Tume inaundwa na Rais, marupurupu ya tume yanawekwa na waziri, kwa watu waaminifu sina shaka kabisa, lakini haiwezi kuwa tume huru wakati stahili zao zinalipwa na watu wa serikali na kuwa na tume kama hiyo wananchi hawatahisi kama wapo huru, anasema.

Anasema Profesa Shivji kuwa katika kifungu cha 9 (2) na (3) kinaeleza kuwa tume itazingatia misingi kamili ya kitaifa na maadili ya taifa kwa kuhifadhi na kudumisha mambo yafuatayo ambayo ni pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kutoa mawazo yao kwa uhuru kwa lengo la kuendeleza na kuboresha masuala hayo.

Upande mmoja unasema wananchi wataweza kutoa maoni yao kwa mambo yote, tume itahifadhi kudumisha mambo hayo ya msingi lakini hata kama mambo ya msingi ndio wananchi wajadili mambo ambayo hawajayataka,” anahoji.
Mapendekezo
Profrsa Shivji anasema Bunge maalum ni chombo muhimu sana katika utunzi wa katiba mpya na linatarajiwa kutoa uhalali wa kisheria na kisiasa hivyo linatakiwa kiwe chombo cha uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi ni vema uangalifu ukawapo na ikatambulika kuwa ni chombo cha wananchi na sio cha umma.

Tume ya katiba ni chombo cha wananchi kiteuliwe moja kwa moja na wananchi bila kujali chama, elimu hadhi na mambo mengine na Mtanzania yeyote ambaye amefikisha umri wa miaka 18 aweze kugombea ujumbe wa Bunge Maalum,” anasema Profesa Shivji.
Anasema Bunge Maalum ni chombo cha wananchi na kura ya maoni ina maana kuwa wananchi wamejadili, wameelewa na wakipotoshwa katika kura za maoni wanaweza kujenga mfumo wa kidikteta.

Ni muhimu sana kutanguliwa na majadiliano ya muda mrefu na ndio maana tulitaka usomwe kwa mara ya kwanza kutoa nafasi ya wananchi kuujadili, lakini muswada huo ambao awali ulisomwa na kufanyiwa mabadiliko umesomwa kwa mara ya pili na mbaya zaidi hata asasi za kiraia tuliupata wiki moja kabla, anasema.

Kuhusu idadi anasema akiwa mwenyekiti wa tume ya ardhi alikuwa na wajumbe 11 na walizunguka nchi nzima, wilaya zote kasoro mbili na anapendekeza wabunge wasizidi 20 na anataka vyuo vikuu na vyama vya kitaaluma kuwa na wawakilishi katika Bunge hilo kwa kuteua watu wawili au watatu ambao wanaona wanafaa kuingia.

Rais anawajibu wa kuchagua wajumbe kutoka katika orodha ndefu ambayo atakuwa ameipata na waziri anaweza kuwa mjumbe wa tume na sekretarieti iundwe na tume yenyewe na wabunge wa bunge hilo la katiba wamchague mwenyekiti wao, malipo na marupurupu yatajwe na sheria yenyewe.
Profesa Shivji anataka asiwepo mtu wa kuwapangia hadidu za rejea wajumbe hao na ziwe kwa mujibu wa sheria zitakazopitoshwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hakuna haja ya hadidu za rejea, majukumu yote ya tume yametajwa sasa kuna haja gani ya hadidu hizo? Tuepuke malumbano na rasimu hiyo itangazwe hadharani kila mwananchi ajue na mwenyekiti wa tume ndiye aiwasilishe rasimu mbele ya Bunge na sio Waziri wa Sheria, anasema.

Kasoro
Kutokana na muundo wa Bunge tulilonalo hao wote wanaingia katika bunge kupitia vyama vyao na mimi ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa sina uwakilishi katika bunge la kutunga katiba na mbaya zaidi asilimia 62 hadi 63 wanatoka chama kimoja, anasema.

Profesa Shivji anasema Bunge la Katiba linalotarajiwa halina tofauti na lile la mwaka 1977 ambalo lilifanya iwepo katiba ya sasa inayohitaji mabadiliko kwani Baba wa Taifa, Rais Julius Kambarage Nyerere aliteua wajumbe kutoka Bunge la Muungano na wale wa Baraza la Mapinduzi.

Kuhusu kura za maoni, Profesa Shivji anasema itatoa uhalali, wengi wakisema NDIO inakuwa na nguvu za kisheria kulingana na wingi wa kura na haiwezi kuwa na uhalali sawa na ule wa uchaguzi mkuu hivyo inapaswa kuelezwa itakuwa imepita kutokana na wingi wa asilimia ngapi.
Kitendo cha kupitishwa kwa wingi wa kura bila kutaja asilimia ni wazi kuwa kuna hatari ya kupitishwa na watu wachache, anasema.

Mwafaka
Profesa Shivji anasema mchakato wa upatikanaji wa kabisa mpya ni fursa muhimu ya kurejesha mwafaka kwa majadiliano kuliko ilivyo sasa ambako kuna kila dalili za kuelekea katika magomvi na mapambano.

Anatoa mfano wa kile kilichotokea Kenya wakati wa mchakato wa katiba mpya ya nchi hiyo na kinachotokea katika nchi zingine na mbaya zaidi anasema nchini Tanzania hayo yanatokea wakati nchi inatajwa kuwa na mgawanyiko wa udini na ukabila.
Profesa Shivji anataka itumike nafasi ambayo inapotea kuweka dira na malengo ya kitaifa.

TeluuDailies: Himalayan viagra

TeluuDailies: Himalayan viagra