Thursday, November 24, 2011

Tume ya katiba sio chombo cha serikali-Shivji


TANZANIA ipo katika vuguvugu la katiba mpya ambalo wiki iliyopita lilichukua sura mpya baada ya matakwa ya asasi za kiraia, wabunge wa vyama vya upinzani na wananchi kwa upande mwingine kupitia asasi za kiraia kupuuuzwa na serikali hivyo kuusoma muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba kwa mara ya pili kinyume na ilivyotakiwa.

Wanaharakati, upinzani na asasi za kiraia walikuwa na hoja ya kutaka muswada huo usomwe kwa mara ya kwanza kwa madai kuwa kuna marekebisho ambayo yamefanywa mara baada ya kusomwa mara ya kwanza na kuusoma kwa mara ya pili si kuwatendea haki wananchi.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu, Profesa Issa Shivji anasema kitendo cha serikali kuusoma kwa mara ya pili na kupuuza hoja za wadau wengine ni jambo lisilofaa na linaweza kuitumbukiza nchi katika matatizo yasiyo na msingi wowote.

Anasema kinachofanyika sasa ni sawa na kile ambacho kilifanyika mwaka 1977 chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa ambapo Rais wa kwanza, Julius Kambarage Nyerere alichagua Bunge la Katiba ambalo liliwashirikisha wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hakuna tofauti na wakati ule hivyo kuna hatari ya kupata katiba ambayo haina uhalali wa wananchi kwani itakuwa imetungwa na watu wachache hivyo sioni kwanini turudie makosa ya miaka 40 iliyopita, anasema.

Akichambua zaidi hoja yake hiyo, anasema kulingana na muswada huo Rais wa Bara atawachagua wajumbe wa tume 36 na ibara ya sita ya muswada huo inaeleza kuwa Rais atachagua wajumbe wengine kwa kutumia vigezo ambavyo vimetajwa baada ya makubaliano na Rais wa Zanzibar na ni pamoja na vile ambavyo Rais ataona vinafaa.

Shivji anasema hapo kuna utata kwani muswada haupo wazi kueleza Rais ataona inafaa vipi na hilo anasema ni kumpa madaraka makubwa kiongozi huyo wa nchi katika uteuzi wa tume hiyo ambayo kimsingi ni ya wananchi na sio ya chama, serikali wala kikundi kingine chochote.

Uteuzi wajumbe wa Tume
Kulingana na muswada huo, wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Baraza la Wawakilishi ambao wapo chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), watakuwa wajumbe wa Bunge hilo la katiba.

Wajumbe wengine wanatajwa kuwa ni mawaziri wa katiba wa serikali zote mbili (Bara/Zanzibar), wanasheria wa pande mbili, wajumbe kutoka mashirika 126 ambayo yameorodheswa na kwa hesabu za haraka Profesa Shivji anasema Bunge hilo litakuwa na wajumbe 554.

Profesa Shivji anasema mchanganuo unaonyesha kuwa wajumbe hao wa Bunge la Katiba kati yao 404 watakuwa wa CCM, 124 watatoka Zanzibar na idadi inayobaki ndio wadau wengine. Profesa Shivji anasema idadi hiyo ni kubwa na haiwezi kuleta ufanisi.
Sijui vipi, lakini India ambayo ina watu wapatao milioni 300 Bunge lao la Katiba mwaka 1945/46 lilikuwa na wajumbe 215 tu, anasema Profesa Shivji.

Swali la kujiuliza hivi wabunge wanaotajwa kuwapo katika Bunge la Katiba wanamwakilisha nani? Wananchi si wapo katika Bunge hilo la Katiba? Je, wao wapo kwa ajili ya nani?
Profesa Shivji anasema makundi hayo mawili yaliingia uwakilishi bungeni kwa mujibu wa katiba iliyopo na walienda huko kutunga sheria kwa mujibu wa katiba hiyo na sio kuipindua ili kuwa na katiba mpya hivyo haoni mantiki ya kuwapo kwao.

Mwenyekiti huyo wa Kigoda cha Mwalimu anahoji kuwapo kwa wabunge wa viti maalum wa CCM na wateule wengine kama asasi za kiraia kunatia wasiwasi na hata hizo NGO ambazo amezichagua Rais si vyombo vya uwakilishi wa wananchi.
NGO ni ‘pressure group’ (makundi ya kushinikiza), tusidanganyane na mara nyingi huwa zinawawakilisha wafadhili baadala ya wananchi. Profesa Shivji anauliza wapi ilipo nafasi ya wananchi katika Bunge hilo?

Aidha anasema kifungu kinachotaja kuwa Rais atateuwa wajumbe baada ya makubaliano na Rais wa Zanzibar ni kuhodhi madaraka ya wananchi.
Kifungu cha sita kimeweka vigezo ambavyo Rais atavitumia na maelezo kuwa na wengine watateuliwa kulingana na vigezo ambavyo rais ataona vinafaa kinajenga maswali zaidi kuliko majibu.

Hapo ni sawa na kumpa mtu kitu kwa mkono wa kushoto kisha kumnyang’anya kwa mkono wa kulia, anasema na kuongeza kuwa Rais kutoa hadidu za rejea za tume hiyo ni kuibaka demokrasia.

Hadidu za rejea
Kulingana na muswada huo, Profesa Shivji anasema kuwa hadidu za rejea zinatolewa na Rais kwa kukubaliana na kushauriana na Rais wa Zanzibar na kitu kama hicho kitafanyika pia katika uteuzi wa katibu wa sekretarieti ya Bunge hilo.
Wajumbe wa sekretarieti watateuliwa na Waziri wa Sheria ambaye pia ndiye mwenye dhamana ya kuwalipa na ndiye ambaye atajua kiwango cha posho na stahili zao zingine na baada ya tume kufanyakazi yake watayakabidhi mapendekezo kwa Rais.

Mapendekezo yatakabidhiwa kwa mujibu wa kifungu namba 18 (2) na baada ya kushauriana na mwenzake wa Zanzibar na baada ya kumaliza majadiliano ya sera na utendaji, Rais atamuagiza Waziri wa Sheria kuwasilisha katika Bunge.
Baada ya kupokea, atamuagiza waziri ayatangaze bungeni, je, akishapokea hataweza kubadili Sheria haimzuii anasema Profesa Shivji.

Shivji anasema anadiriki kusema kuwa ni tume ya marais wawili wa Zanzibar na Bara na sio ya katiba na anaeleza hatua ya kwanza katika kuiunda imewaacha wananchi kando hivyo kupotosha mchakato mzima.
Mwenyekiti huyo wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere anasema sekretarieti ni muhimu ni nani anaiteua ni jambo ambalo linahitaji umakinifu mkubwa na anatoa mfano wakati alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Sheria ya Ardhi wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi.

Nilipochaguliwa kuwa mwenyekii wa tume ya ardhi na kupewa ofisi Wizara ya Ardhi, sekretarieti ilikuwa itoke Wizara ya Ardhi, watumishi wa wizara ndio walikuwa sekretarieti, mkutano wa kwanza na wa pili tulioufanya, miniti za kikao hazikuchuliwa, hapo nikaona wazi kuwa tume haiwezi kufanyakazi.

Anasema aliona hivyo kutokana na ukweli kuwa huwezi kuwa na seretarieti kutoka wizarani ambao ndio wanaochunguzwa na tume jambo ambalo alililalamikia na kutakiwa kuchagua sekretarieti yake mwenyewe, hali ambayo ilimuwezesha kufanya kazi zake inavyotakikana.
Tume inaundwa na Rais, marupurupu ya tume yanawekwa na waziri, kwa watu waaminifu sina shaka kabisa, lakini haiwezi kuwa tume huru wakati stahili zao zinalipwa na watu wa serikali na kuwa na tume kama hiyo wananchi hawatahisi kama wapo huru, anasema.

Anasema Profesa Shivji kuwa katika kifungu cha 9 (2) na (3) kinaeleza kuwa tume itazingatia misingi kamili ya kitaifa na maadili ya taifa kwa kuhifadhi na kudumisha mambo yafuatayo ambayo ni pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kutoa mawazo yao kwa uhuru kwa lengo la kuendeleza na kuboresha masuala hayo.

Upande mmoja unasema wananchi wataweza kutoa maoni yao kwa mambo yote, tume itahifadhi kudumisha mambo hayo ya msingi lakini hata kama mambo ya msingi ndio wananchi wajadili mambo ambayo hawajayataka,” anahoji.
Mapendekezo
Profrsa Shivji anasema Bunge maalum ni chombo muhimu sana katika utunzi wa katiba mpya na linatarajiwa kutoa uhalali wa kisheria na kisiasa hivyo linatakiwa kiwe chombo cha uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi ni vema uangalifu ukawapo na ikatambulika kuwa ni chombo cha wananchi na sio cha umma.

Tume ya katiba ni chombo cha wananchi kiteuliwe moja kwa moja na wananchi bila kujali chama, elimu hadhi na mambo mengine na Mtanzania yeyote ambaye amefikisha umri wa miaka 18 aweze kugombea ujumbe wa Bunge Maalum,” anasema Profesa Shivji.
Anasema Bunge Maalum ni chombo cha wananchi na kura ya maoni ina maana kuwa wananchi wamejadili, wameelewa na wakipotoshwa katika kura za maoni wanaweza kujenga mfumo wa kidikteta.

Ni muhimu sana kutanguliwa na majadiliano ya muda mrefu na ndio maana tulitaka usomwe kwa mara ya kwanza kutoa nafasi ya wananchi kuujadili, lakini muswada huo ambao awali ulisomwa na kufanyiwa mabadiliko umesomwa kwa mara ya pili na mbaya zaidi hata asasi za kiraia tuliupata wiki moja kabla, anasema.

Kuhusu idadi anasema akiwa mwenyekiti wa tume ya ardhi alikuwa na wajumbe 11 na walizunguka nchi nzima, wilaya zote kasoro mbili na anapendekeza wabunge wasizidi 20 na anataka vyuo vikuu na vyama vya kitaaluma kuwa na wawakilishi katika Bunge hilo kwa kuteua watu wawili au watatu ambao wanaona wanafaa kuingia.

Rais anawajibu wa kuchagua wajumbe kutoka katika orodha ndefu ambayo atakuwa ameipata na waziri anaweza kuwa mjumbe wa tume na sekretarieti iundwe na tume yenyewe na wabunge wa bunge hilo la katiba wamchague mwenyekiti wao, malipo na marupurupu yatajwe na sheria yenyewe.
Profesa Shivji anataka asiwepo mtu wa kuwapangia hadidu za rejea wajumbe hao na ziwe kwa mujibu wa sheria zitakazopitoshwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hakuna haja ya hadidu za rejea, majukumu yote ya tume yametajwa sasa kuna haja gani ya hadidu hizo? Tuepuke malumbano na rasimu hiyo itangazwe hadharani kila mwananchi ajue na mwenyekiti wa tume ndiye aiwasilishe rasimu mbele ya Bunge na sio Waziri wa Sheria, anasema.

Kasoro
Kutokana na muundo wa Bunge tulilonalo hao wote wanaingia katika bunge kupitia vyama vyao na mimi ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa sina uwakilishi katika bunge la kutunga katiba na mbaya zaidi asilimia 62 hadi 63 wanatoka chama kimoja, anasema.

Profesa Shivji anasema Bunge la Katiba linalotarajiwa halina tofauti na lile la mwaka 1977 ambalo lilifanya iwepo katiba ya sasa inayohitaji mabadiliko kwani Baba wa Taifa, Rais Julius Kambarage Nyerere aliteua wajumbe kutoka Bunge la Muungano na wale wa Baraza la Mapinduzi.

Kuhusu kura za maoni, Profesa Shivji anasema itatoa uhalali, wengi wakisema NDIO inakuwa na nguvu za kisheria kulingana na wingi wa kura na haiwezi kuwa na uhalali sawa na ule wa uchaguzi mkuu hivyo inapaswa kuelezwa itakuwa imepita kutokana na wingi wa asilimia ngapi.
Kitendo cha kupitishwa kwa wingi wa kura bila kutaja asilimia ni wazi kuwa kuna hatari ya kupitishwa na watu wachache, anasema.

Mwafaka
Profesa Shivji anasema mchakato wa upatikanaji wa kabisa mpya ni fursa muhimu ya kurejesha mwafaka kwa majadiliano kuliko ilivyo sasa ambako kuna kila dalili za kuelekea katika magomvi na mapambano.

Anatoa mfano wa kile kilichotokea Kenya wakati wa mchakato wa katiba mpya ya nchi hiyo na kinachotokea katika nchi zingine na mbaya zaidi anasema nchini Tanzania hayo yanatokea wakati nchi inatajwa kuwa na mgawanyiko wa udini na ukabila.
Profesa Shivji anataka itumike nafasi ambayo inapotea kuweka dira na malengo ya kitaifa.

No comments: