Wednesday, March 24, 2010

• Akabiliana na shinikizo kutoka Kigoma, Geita

UAMUZI wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kutangaza azma yake ya kufanya kile alichokiita utafiti wa kujua ni jimbo gani agombee kati ya matano aliyoyaainisha unaonekana kumuweka katika mazingira magumu kisiasa; Tanzania Daima limebaini.

Majimbo hayo matano ambayo tayari yanaonekana kuanza kumgonganisha kichwa Zitto kwa upande mmoja na viongozi na wanachama wa kawaida wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa upande mwingine ni Geita, Kahama, Kigoma Kaskazini, Kigoma Mjini na Kinondoni.

Matukio ya hivi karibuni yanayoweza kumuweka njia panda Zitto ni lile la kuwapo kwa taarifa za vyombo vya habari zinazoonyesha kuwapo kwa shinikizo kutoka kwa wazee wa Kigoma anakotoka mwanasiasa huyo kijana la kumtaka aachane na mipango yake ya kutaka kugombea jimbo lolote nje ya mkoa huo.

Habari iliyoandikwa na gazeti moja la kila siku (siyo Tanzania Daima) ambalo kwa muda mrefu sasa limekuwa na mwelekeo wa kumjenga kisiasa Zitto zinaeleza kuwa wazee wa Kigoma wameshtushwa na hatua ya kijana wao huyo kuanza kusaka jimbo la kugombea.

Wakati wazee wa Kigoma wakitoa tamko hilo, habari kutoka Geita zinaeleza kuwa wakazi wa eneo hilo wameanza kuchangishana fedha zinazofikia sh 50,000 zitakazomwezesha Zitto kuchukulia fomu za kugombea huko.

Katibu wa CHADEMA wilayani Geita, Rogers Luhega, aliliambia Tanzania Daima kwa njia ya simu jana kuwa uamuzi wa kumtaka mwanasiasa huyo kugombea ubunge kwao ulijadiliwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji cha jimbo hilo kilichoketi hivi karibuni.

Luhega alisema uamuzi wa kumpendekeza Zitto kuwa mgombea pekee wa ubunge katika jimbo hilo uliwasilishwa ofisini kwake kwa njia ya barua iliyokusanya maoni ya wana CHADEMA kutoka kata 11 zilizomo jimboni humo.

“Haya ni maombi ya kata zote zilizopo Geita ambazo zilifikia uamuzi huo Machi 14 mwaka huu na kutoa mapendekezo haya ambayo pamoja na mambo mengine yanataka Zitto ateuliwe kuwa mgombea pekee,” alisema.

Alibainisha kuwa kutokana na maombi hayo, CHADEMA wilaya imeshamuandikia barua Zitto, yenye kumbukumbu namba CDM/GT/2010 ikimjulisha kile kilichopendekezwa na wanachama.

Akizungumza kwa simu na Tanzania Daima jana, Zitto alikiti kupokea barua hiyo na mara moja akawataka wana CHADEMA hao wa Geita kuwa na subira.

“Tayari nimeipokea barua ya kuombwa kuwa mgombea pekee nafasi ya ubunge jimbo la Geita mjini kupitia CHADEMA, nafurahi kwa heshima hii, siwezi kukataa lakini ninachowaomba wakazi wa Geita ni kuwa na subira ili nikamilishe taratibu zote ndani ya chama,” alisema Zitto.

Zitto alisema jambo hilo ni kubwa na si busara kulitolea kauli au uamuzi katika kipindi hiki ambacho bado hajaamua ni jimbo gani anapaswa kuwania ubunge.

Alibainisha kuwa alikuwa akikusudia kutoa uamuzi wake Jumamosi hii ya Machi 27 wakati wa mkutano wa Kamati ya Utendaji ya CHADEMA uliopangwa kufanyika mkoani Dodoma.

Jimbo la Geita ambalo linaongozwa na Ernest Mabina kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kipindi cha miaka 10 katika siku za hivi karibu limeonekana kuwa na ushindani mkubwa kati ya CCM na CHADEMA.

Umaarufu wa Zitto katika majimbo ya Geita na Kahama yenye utajiri wa dhahabu, kwa kiwango kikubwa yalijengwa tangu mwanasiasa huyo alipoibua kashfa ya mkataba wa madini wa Buzwagi miaka mitatu iliyopita.

Hata hivyo, nafasi ya Zitto kutoa uamuzi huo Jumamosi hii ni finyu kutokana na chama hicho kufikwa na msiba wa kiongozi wake wa juu, Mzee Christopher Ngaiza, aliyefariki Nairobi, Kenya mwishoni mwa wiki.

Hatua ya Zitto kulazimika kusaka jimbo la kugombea na hususan ule wa kuonekana akibadili uamuzi wa kuendelea kugombea Kigoma Kaskazini umekuwa ukichochewa na mabadiliko ya hali ya hewa kisiasa kwa upande wake.

Kiongozi mmoja wa CHADEMA aliyezungumza na gazeti hili alisema, suala la Zitto kubadili mwelekeo wa kutaka kuendelea kuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kulianza kujengwa miaka takriban mitatu iliyopita alipokaririwa na gazeti hili akisema alikuwa hana mpango wa kugombea ubunge mwaka 2010.

Tamko hilo la Zitto ambalo liliibua mshtuko mkubwa ndani na nje ya CHADEMA, lilifuatiwa na lile lililotolewa bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akimtaka mbunge huyo kijana kuwa makini asije akashtukia amepoteza jimbo hilo.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Pinda alitoa tamko hilo siku chache tu baada ya kufanya ziara mkoani Kigoma ambako pamoja na mambo mengine alizindua barabara muhimu inayopita katika Jimbo la Kigoma Kaskazini.

Mbali ya hayo, kuwapo kwa taarifa kwamba moja ya kata muhimu yenye wapiga kura 15,000 ya Mwandiga iliyoko katika Jimbo la Kigoma Kaskazini itahamishiwa katika jimbo la Kigoma Mjini, kumekuwa kukitajwa hata na Zitto mwenyewe kuwa sababu iliyomfanya afikirie mara mbili mbili kurejea huko.

Kuhamishwa kwa kata ya Mwandiga yenye wanachama wengi wa CHADEMA kwenda Kigoma Mjini kumewafanya wengi kuanza kuona nafasi ya kijana wao kuendelea kuwa mbunge ikihamia pia katika jimbo hilo.

Hata hivyo, habari zinaeleza kuwa, Zitto mwenyewe amekuwa akisita kugombea Jimbo la Kigoma Mjini kutokana na kukwepa kujiingiza katika mzozo wa kisiasa na Mbunge wa sasa wa CCM, Peter Serukamba, ambaye wana uhusiano wa kihistoria wa kifamilia.

Mkanganyiko huo, habari zinaeleza, ulimfanya mwanasiasa huyo aamue kimsingi kulipa jimbo la Kinondoni chaguo lake la kwanza na kuyaacha mengine manne yakifuatiwa kutegemea na upepo wa kisiasa utakavyovuma.

Source: Tanzania Daima

1 comment:

Anonymous said...

Right until 1950 Janie existed want a take up residence power storage facility.
Which has an hawaiian mug of coffee photos community coffee shop?
Write-up put a look modest face and head of the residence.
It's always best to decrease at least one tsp . with regard to water.

Also visit my homepage vacuum coffee pot suppliers