Friday, September 05, 2014
Namna mahitaji ya kihisia ya wenzi yanavyosababisha misuguano ya kimahusiano na ndoa
PAMOJA na dini nyingi kubwa kupiga marufuku talaka kwa waumini wake, takwimu rasmi za Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) zinaonyesha kwamba talaka nchini zimeongezeka kwa asilimia 49 katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2009. Kwa upande wa Zanzibar pekee, tunaambiwa, asilimia 95 ya migogoro 1,753 ya ndoa iliyosajiliwa kwenye Mahakama ya Kadhi nchini humo iliishia kwa talaka. Hali inatisha, au sio?
Katika hali halisi, shauri ya utamaduni wa kuyaonea aibu masuala ya kuachana, hali inaweza kuwa mbaya zaidi. Watu wengi wanaweza kuwa wanaugulia maumivu ya ndoa na kuamua ama kufa na tai shingoni, au kutafuta 'michepuko' ya hapa na pale katika jitihada za kupunguza maumivu.
Katika nchi za Ulaya, ambako kidogo kuna uhuru wa mtu kufanya atakalo ikiwa ni pamoja na kuomba talaka, hali ni tete zaidi. Kwa mfano, tunaambiwa, wakati idadi ya ndoa zinazofungwa mwaka 2010 ilipungua kwa asilimia 39 barani humo, talaka zimeongozeka kwa asimilia 200 katika kipindi cha mwaka 1979 mpaka 2010.
Takwimu hizi zinaonyesha namna taasisi ya ndoa inavyoendelea kupoteza umaarufu wake kwa kasi huku watoto wengi wakiendelea kuzaliwa nje ya ndoa. Katika nchi nyingi za Ulaya, asilimia zaidi ya 50 ya watoto wanazaliwa nje ya ndoa. Iceland oekee kwa mfano, asilimia ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa imefikia 66.9 mwaka 2012. Hapo hatujazungumzia mimba zilizotolewa pamoja na kukithiri kwa matendo ya uzinzi na uasherati ambayo ni matokeo ya michepuko ya wanandoa waliochoka maisha ya ndoa.
Ingawa jambo hili limekuwa likifanyiwa utafiti tangu zamani, kwa sasa limeanza kuvutia hisia za watafiti wengi zaidi kufuatia ongezeko hilo la talaka. Jambo linalohitaji majibu ya hakika na makini ni kwamba iweje wapenzi wanaoanza mapenzi yao kwa msisimuko kujikuta katika hali ya kuchokana na hata kuachana katika kipindi kifupi? Kwa nini wapenzi waliooana kwa 'harusi ya kufa mtu', kwa furaha na nderemo za matumaini makubwa, wajikute wakizozana kwa hasira na uchungu, wakipigana, kupishana, kuchokana na hata kufikia kuhisi suluhu pekee ni ama 'kuchepuka', 'nyumba ndogo' au kuachana rasmi? Tumekosea wapi? Kwa nini ndoa inazidi kuwa taasisi iliyo kwenye hatari ya kupotea?
Tafiti zinasemaje kuhusu mitazamo ya wanandoa wanaotengana?
Utafiti uliofanywa na Amato na Previti na kuchapishwa kwenye Jarida la Masuala ya Familia mwaka 2003, unaonyesha kwamba watu wengi wanaachana kwa sababu ya hisia za kukosekana kwa uaminifu, wenzi kushindwa kuwasiliana, hisia za kukosekana mapenzi na hivyo wenzi kujikuta wakijisikia watu wasio na furaha tena na mengine mengi.
Tafiti za awali zimefanya jitihada ya kujua sababu za kuchokana huko kwenye ndoa kwa kutazama makundi mbalimbali. Tukianza na jinsia, watafiti Levinger; Cleek & Pearson; Kitson; Bloom, Niles & Tatcher kwa nyakati tofauti walichunguza mitazamo ya wanaume na wanawake kuhusu sababu ya migogoro. Wanaume wanaorodhesha sababu kama vile wanawake kuwa wazinzi na kutumia muda mwingi kazini kuliko nyumbani, kukosekana mawasiliano baina ya wenzi, kubadilika kwa vipaumbele, kama sababu kuu.
Wanawake kwa upande wao wanataja ulevi na uzinzi wa wenzi wao wa kiume; mwanaume kushindwa kuihudumia familia yake kifedha; udhalilishaji wa kihisia na kimwili hali inayosababisha furaha kutoweka na kutokuendana kitabia kama tatizo kuu.
Kadhalika, tafiti nyingine zilizofanywa na Kitson, Levinger na Goode kwa nyakati tofauti, zimejaribu kutazama uwezo wa kifedha na elimu katika matatizo haya.
Ndoa na mahusiano ni mada inayouza vitabu kwa wingi Picha
msome zaidi bwaya
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Nice blog and article, thanks for sharing.
Post a Comment